Header Ads

Responsive Ads Here

WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI NCHINI WAMPONGEZA RAIS MAGUFULI KUBAINI MABILIONI YA HASARA ITOKANAYO NA MCHANGA WA MADINI.


MADIN
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimba Madini Nchini (FEMATA), John Bina (katikati) akitoa pongezi za shirikisho kwa Rais Dkt.Magufuli kwa hatua yake ya kubaini hasara ya mabilioni ya fedha iliyokuwa kisababishwa na mchanga kusafirishwa nje ya nchi. Kulia ni Mwenyekiti wa Wachimbaji Madini Wadogo Mkoa wa Singida Robert Marando na kushoto ni Mtendaji Mkuu wa FEMATA Haroun Kinega.

………………………………………………………..
Na Nathanie Limu- Singida
Wachimbaji wadogo wa madini nchini wamempongeza Rais WA Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kubaini nchi inavyopata hasara ya mabilioni ya fedha kutokana na usafirishaji wa machanga wenye madini nje ya nchi.
Pongezi hizo zimetolewa na Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimba Madini (FEMATA) Tanzania John Bina wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano wa hotel ya Stanley Motel mjini Singida.
Amesema wamefikia uamuzi huo wa kutoa pongezi kwakuwa Rais Magufuli ameonyesha uthubutu wa aina yake na uzalendo wa kweli kwa taifa la Tanzania.
“Taifa limeingia hasara kubwa kutokana na mbinu chafu iliyotumika kusafirisha mchanga wenye madini nje ya nchi. Mchanga huu tuliaminishwa kuwa ni mchanga mtupu hauna madini kumbe ndani yake kuna madini mbalimbali. Kwa ushupavu mkubwa rais wetu kupitia kamati aliyoiunda ameweka hadharani ukweli kuhusu nchi ilivyokuwa ikiibiwa”, amefafanua Bina.
Amesisitiza kuwa Rais Magufuli anastahili pongezi za kipekee kwa hatua aliyochukua na anapaswa kuungwa mkono na Watanzania wote wazalendo.
“Kutoka kwenye sakafu ya moyo wangu, na wachimbaji madini wadogo nchini, tunamuunga mkono rais wetu kwa kuonyesha uzalendo wa hali ya juu katika kulinda rasilimali zetu. Sio kulinda tu, tutahakikisha shughuli zetu zinakuwa za uwazi na tutatii sheria za madini, bila kushurutishwa”, amesema.
Ameongeza kuwa, “Mungu amjalie nguvu na afya rais wetu aendelee na ujasiri wa kuziba mianya yote inayoliingiza Taifa hasara za kutisha”.
Bina amesema taifa limeumia mno kutokana na mabilioni ya fedha kupotea miaka yote hiyo, rais ameonyesha ukomavu wa hali ya juu kwa vitendo vyake vya kusimamia kile anachokiamini.
“Kwa pongezi hizi sisi wachimbaji wadogo sio kwamba tunawachukuia wachimbaji wakubwa wakiwemo wanaosafirisha mchanga nje ya nchi, hapana. Kupitia kwao tumejifunza mambo mengi lakini kwa hili la kulitia hasara taifa letu hatukubaliani nao. Tunapenda wawe wa kweli na wakati wote watoe taarifa zenye ukweli mtupu”, amesema rais Bina.
Amesema makampuni makubwa yana uzoefu mkubwa kutokana na kufanya shughuli za uchimbaji madini kwa miaka mingi hivyo wana mbinu nyingi nzuri na pia za uhujumu hazikosekani.
Katika hatua nyingine rais Bina ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wachimbaji wadogo wajibu wa kulipa kodi na malipo ya mirahaba bila kushurutishwa.
Pia ameishauri serikali kuangalia uwezekano wa kununua kinu/tanuru (smeltler) cha kuchomea madini hata kwa kukopa ili kuziba mwanya wa mchanga kusafirishwa nje ya nchi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa wachimbaji madini mkoa wa Singida, Robert Marando pamoja na kupongeza hatua ya rais Magufuli amewakumbusha wachimbaji kutii sheria za madini na kulipa stahili za serikali ili kuijengea uwezo serikali iweze kutoa huduma muhimu kwa wananchi kwa ufanisi.
Naye Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la FEMATA, Haroun Kinega amesema wachimbaji wote wa madini nchini, waungane na kushirikiana kutekeleza kwa dhati maagizo yote ya rasi Magufuli ili rasilimali madini iweze kutoa mchango unaostahili katika maendeleo ya nchi.

No comments