Header Ads

Responsive Ads Here

USHIRIKA WA ‘SUBIRA NJEMA’ WA WATU WENYE ULEMAVU MIAKA NANE MFULULIZO WATENGEZA SABUNI KWA MKONO

WANAKIKUNDI cha upakasaji mikoba, makawa, vipochi vya ukili na upandaji miti cha ‘Subira njema’ kilichopo kijiji cha Changaweni Wilaya ya Mkoani Pemba, ambao wengi wao ni watu wenye ulemavu, wakiwa kazini katika kazi yao hiyo ambapo mkoba mmoja wa kisasa wenye zipu ni shilingi 20,000 hadi shilingi 25,000, (picha na Haji Nassor, Pemba)
WAJASIRIAMALI kisiwani Pemba, wakiwa na sabuni za michi, nje ya ukumbi wa kiwanda cha mafuta ya Makonyo Wawi Chakechake baada ya kuhitimu mafunzo hayo, (Picha na Haji Nassor, Pemba)


NA HAJI NASSOR, PEMBA

“………kozi mwana mandanda kulala na njaa kupenda…………..”

Huu ni msemo maarufu ambao unatumika katika visiwa vya Unguja na Pemba na hata kuleTanzania bara kwa baadhi ya maeneo.

Hapo zamani za kale, wazee wetu walikuwa wanapenda zaidi kutumia misemo kuliko bakora, kwa lengo la kuwafundisha na kuwaasa wanaowalea

‘’Maskini enzi zetu zimeshapita ‘’baadhi ya wazee wenye umri wamekuwa wakisema kwa karne hii.

Katika zama hizi za Sayansi na Teknologia, si wengi ambao wanajua maana ya misemo kadhaa, bali wengi wanaisikia tu na kutokua na jawabu rasmi.

Kwa hapo zamani misemo ni miongoni mwa bakora inayoweza kutumika kupiga mtu na mwenye akili timamu.

Ilikuwa kwa hapo karne hiyo, misemo, inaweza kujua kwamba muda gani mtu anatakiwa afanye nini, au ache kufanya jambo fulani, na kuwepo kwa matunda.

‘Ama kweli lishalo vuusha sidau’’, ndio maana leo hii waliowengi hawathamini na wala hawajali misemo mbali mbali ya wazazi wetu ambao ndio waliotuzaa. 

Nisiende mbali naogopa nisije nikageuka muazima jamvi…….. kwa wale wanaofahamu ni kwamba mara husau lengo alilokwendea kwa jirani.

Nami hapa naogopa na naheshimu nisije nikalisahau lengo langu ndani ya waraka huu wa makala ambayo kwa hakika imenivutia na ndio maana nikaamua kuiandika.

Lengo hasa ni kikundi cha ushirika cha wanawake tena wenye ulemavu kilichopo kijiji cha Changaweni wilaya ya Mkoani ndani ya Kisiwa cha marashi ya karafuu.

“Ile kauli isemayo………. wanawake wanaweza hapa haikwenda kombo kwa wanawake hawa ukizingatia wao ni wenye ulemavu”, ni kweli kabisa wanaweza.

Si wengine bali ni wanaushirika wa” Subira njema” wanawake ambao ni walemavu na hapa nilitaka kujua historia ya wanaushirika hawa.

Nilianza kuweka kalamu na shati langu sawa, wakati nikizungumza na Amina Abdalla Said, yeye ndie Mwenyekiti wa wanaushirika hao.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, ushirika wao ambao wanajituma usiku na mchana kwa lengo lakupata riziki zao za halali, unajishughulisha na kazi mbali mbali.

‘’Sisi hapa twapakasa mikoba ya ukili lakini hii ya kisasa, nikamuliza hata mikoba ya ukili kuna ya kisasa kumbe? akajibu ndioo huku akicheka.


Ushirika huo wa wanawake wenye ulemavu ulianza mwaka 2009, ukiwa na wanachama 10 wakiwemo wanaume wawili.

Kwa sasa unajishughulisha zaidi na utengenezaji wa sabuni za kufulia, kuoshea vyombo na kuogea na vipochi vya ukili.

Mwenyekiti akizungumza na mwandishi wa makala haya, hapo Changaweni Mkoani, hakuacha kuniambia kuwa wanatengeneza sabuni, je wanayo mashine.

Suali hili nilimtupia tena Mwenyekiti huyo na bila ya kusita, akasema kuwa ‘tunatumia mikono na ndoo na hatuvai hata ‘glavu’ yaani kukinga ngozi’’,alisema.

Hili linatokana na kutokuwa na vifaa vya kutengenezea sabuni na kukumba na kemikali kadhaa ikiwa ni pamoja na ile ya ‘kastik’ ambayo huichanganya na malighafi nyengine.

Salama Mwadini Juma ambae ni mwanachama wa ushirika huo wa ‘’Subira njema‘’ anasema hili hasa la kukosa mashine, limekuwa likiwahatarishia usalama wa afya zao.

Anaona kuwa, licha uzalishaji huo kuwa ni muda mrefu, lakini hadi sasa hawajapatiwa mashine na kuendelea kuzalisha sabuni kwa kutumia mikono.

Akizungumzia suala la soko la bidhaa hiyo Mshika fedha wa ushirika Nassra Yussuf Khalifan, bado halijanyanyuka vyema, na wamekuwa wakiuza kwa kubahatisha.

‘’Kwa sasa wateja wetu ni hawa wanaokuja hapa hapa na kujinunulia, lakini lile soko kubwa halipo, lakini pia kwa sababu bidhaa haziko kwenye kiwango’’,alisema.

Ushirika huo kwa sasa hauna ‘pekingi’ ya biashara zao, jambo ambalo huwenda ikawa ni sababu moja wapo ya kutokuwa na soko la hali ya juu.

Miongoni mwa aina sabuni wanazotengeneza kwa kutumia malighafi za mchachai, mkaratusi, na nyengine baada ya kupewa mafunzo kupitia Umoja wa watu wenye Ulemavu Zanzibar UWZ.

Ushirika huu, kwa muda wa miaka nane sasa wanaendelea kuweka maisha yao rehani, kwa kuendelea kutumia mkono yao kutengeneza sabuni kw aukosefu wa mashine.

Soko la uhakika hasa la bidhaa ya sabubu ndani ya ushirika huu, bado ni kizungumkuti, maana hulazimika kuzikopesha ili zisijewaharibikia mikononi mwao.


Sabuni zenye thamani ya shilingi 150,000 sawa na michi 50 ya sabuni ziko mikononi mwa wateja wao, maana hawana soko la uhakika na vyenginevyo wakiogoa kuzikopesha ndio hawafikii malengo.

Hivi karibuni kwa kutumia mikono yao, walizalisha sabuni boksi tano na kila moja, huingiza michi 25, ambapo boksi tano zenye michi 75 sawa na shilingi 225,000 walibahatika kuziuza. 

Mbali na mambo hayo ya usafi na povu, lakini ushirika huu ulionzishwa mika nane iliopita, unajishughulisha na utengenezaji wa mikoba ya kisasa na vipochi vya ukili ,mikeka na makawa .

Kwenye ushirika huu wanauza mkoba mmoja kwa bei ya shilingi 10,000 hadi shilingi 15,000 kutokana na ukubwa wa mkoba huiska.

‘Lakini pia ipo mikoba mengine hii ambayo sio ya kileo sana hii tunauza kati ya shilingi 8,000 hadi shilingi 7,000 alisema huku akiwa na mkoba mkononi Nassra Yussuf.

Kwa kwenye ushirika huo, pia kwa vile wajishughulisha na upakasaji wa makawa, huwezi kulipata kama huna shilingi shilingi 3,500 au shilingi 4,000.

Ukija kwenye zulia la usumba ambapo ushirika huu unatengeneza na kuliuza kati ya shilingi 7,000 kwa moja, wakati mkeka mmoja ni wenye ukubwa ni shilling.40,000.

Ushirika huo wa wanawake baada ya kuhangaika huku na kule, kwa sasa umeshaweka mikono yake wazi kwenye benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) kwa kuwa na ‘Account’ namba 041207000765.

Kwa mujubu wa mshikafedha wa ‘Subira njema’ Nassra anabainisha pia kibakuli chao hicho hakiko kitupa maana kina akiba ya zaidi ya shilingi laki tano (500,000).

Toka kuanza ushirika huo hadi sasa, hawajawahi kupata msaada wowote kutoka Serekalini, ingawa wameshaomba mara kadhaa.

Jambo hilo linawashangaaza sana maana walitakiwa kuanzisha vikundi vya aina hiyo, lakini kwa sasa mambo ni magumu, kwao kutokana na kuwa hawakumbukwi.

‘’Maisha ni safari refu na safari ni hatua ‘’, na hatua lazima unyanyue mguu lakini sisi mguu wetu umekwama na tunahitaji kukwamuliwa’’, alifafanua Mshikafedha huyo.

Sikutosheka na hayo nilitaka kujua changamoto ambazo zimewakabili, ili kuweza kujua jinsi ya kuwasaidia kupitia ukurasua huu.

Salama Mwadini Juma ambae ni mjumbe katika ushirika huo wa wanawake wenye ulemavu hakunyamaza kimya, akasubiri kila kitu kusemewa alinyanyua mdomo tena kwa sauti akiwa na tamaa kubwa ya kupata msaada. 

Bi Salama anasema kuna changamoto mbali mbali ambazo zimewakabili katika ushirika wao, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vitendea kazi. 

‘’Ofisi hatuna, sabuni mapaka leo twafanyia mikono, soko madhubuti ambapo haya yanatukwaza sana’’,alieleza huku akiwa na masikitiko.

Asya Ali Hamadi, ambaye nae ni mjumbe katika ushirika wa ‘’Subira njema‘’ suala la kufanyia sabuni ndani ya nyumba ya mwanachama ni hatari hata kiusalama wa watoto wao.

Aliomba Serekali kupitia Wizara ya Uwezeshaji kuwaangalia kwa jicho la huruma, kwani wakiwapatia msaada wataweza kujiendeleza zaidi. 

Lakini aliwageukia wanawake wenzake wale ambao hawajishughulishi na chochote, wajitume na waondokane na dhana ya kuwa mwanamke siku zote ni mtu wa kukaa ndani.

Akasema hiyo ni dhana potofu, na anaetaka kujua juu ya hilo afike ‘Subira njema’ Changaweni, kwani wanawake wanaweza hata kama hawakuwezeshwa.

Ndio hapa pakuanzia kwa Wizara yetu ya uwezeshaji, kwani kwa muda mrefu wanawake walionekana hawawezi ndio maana wakabakia majumbani na kuhudumia watoto.

Asha Hassan Makame, ambae hajajiingiza kwenye kikundi chochote cha ushirika, anasema natamani sana ingawa, changamoto anayoiona ni kutengwa kwa kukoseshwa vifaa.

“Vipo vikundi vingi vya wanawake, lakini huona kama vile maisha yao hayajabadilika yako sawa na yangu, sasa Napata wasiwasi wa kujiunga na mimi’’,anasema.

Ingawa Maulid Saleh Hamad wa Kiuyu yeye anasema kama yupo mwanamke Tanzania hii hajajiunga na wala hanadhamira ya kujiingiza kwenye ushirika amechelewa.

Mratibu wa TAMWA Zanzibar Mzuri Issa, yeye anaona ili uwanaharakati wa mwanamke utimie ni kukusanya nguvu zao pamoja.

“Baada ya lazima sasa serikali ione umuhimu wa kuwasaidia vifaa kama hao wanawake wenzetu wa Changaweni, ili wasonge mbele’’,alifafanua.

Mlekwa Makame Hija wa Mkoani, anasema kama wanawake wakishajiunga pamoja na kusaidiwa vifaa, wanaweza kupiga hatua moja kubwa ya kimaendeleo.

Ingawa sheikh Nassor Khamis wa Mizingani anasema lazima wanawake waliopata ruhusa kwa waume zao, kujiingiza kwenye vikundi hivyo, wasisahau wajibu na majukumu yao, kama walivyo kwa wanaume.

Mkuu Wa mkoa wa kusini Pemba, Mwanajuma Majid Abdalla anasema jambo la kwanza ni mwanamke kukubali kujiingiza kwenye njia za kujikomboa.

“Unajua serikali na hata wafadhili hupenda zaidi kuwasiaidia wanawake waliojikusanya, sasa lazima tuhamasishahe kuefanya hivi, ili tujikomboe’’,anashauri.

Naibu Katibu mkuu wozara inayoshughulikia wanawake na watoto Mauwa Makame Rajab ameutaka uongozi wa ushirika huo, wasisite kufika wizarani ili kupata ufumbuzi.

“Waende wizarani baada ya kujua gharama ya mashine ya kutengeneza sabuni, kisha wanaweza kupewa maelekezo ya kuandika barua na kuomba mkopo’’,anashauri.

Anesema haipendezi na ni hatari kushika kemikali kwa mikono wakati wanajikomboa kwa kutengeneza, sabuni waombe mkopo wanunue mashine. 

Shemsa Hakim Khamis ambae amejiari kwenye gari ya TAX eneo la uwanja wa ndege Pemba, anasema lazima wanawake sasa wawe na njia ya kujikomboa.

“Maisha sasa yapaa, lazima kila mmoja ndani ya familia awe chanzo cha mapato, ili kuimarisha ndoa na familia’’,alishauri

Kwa upande wake mjasiriamali anaejishughulisha na ususi wa mikoba ya kisasa, wa Kiuyu wilaya ya Wete Nassra Salim Mohamed anasema hata kama mwanamke ameolewa, lakini kujiingiza kwenye uwanaharakati ni lazima.

Asha Muhidin Mjaka wa Wawi ambae hajajiingiza kwenye ujasiriamali, anasema bado hajapata elimu ya juu ya jambo hilo.

“Mimi sijapa elimu na ndio maana hadi sasa naendelea na kilimo cha migomba, mihogo na mpunga peke yangu’’,alisema.

Mwakilishi wa jumuia ya watu wenye ulemavu Zanzibar UWZ Pemba Salum Abdallah, amekitaka kikundi hicho cha ususi wa mikoba kuwashirikisha ili kuwatafutia mashine.

“UWZ ipo kwa ajili ya kuwahudumia wanachama wake, sasa wanapokwama waje ili tuone wanaendeleza njia yao ya kujikomboa’’,alishauri.

Daktari Makame Hassan Makame, anasema kemikali na mchanganyiko wa dawa nyengine zikiingia kwenye ngozi ya mwanadamu husababisha madhara kadhaa.

“Moja ni ngozi kukosa hisia unaweza kuungua moto ukachelewa kufahamu, lakini pia ngozi kukosa kuhifadhi mafuta’’,alisema.

No comments