Header Ads

Responsive Ads Here

USAFIRISHAJI HATARISHI WA MAZAO YA MISITU NI CHANZO CHA AJALI, UKWEPAJI KODI NA UHARIBIFU WA MISITU.


Jovina Bujulu- MAELEZO.
Misitu  ni ardhi yoyote yenye uoto wa mime na wingi wa miti iwe ya asili au ya kupanda yenye kimo chochote, ivunwayo na isiyonunwa  na iliyo na uwezo wa kutoa mbao au mazao  mengine yenye uwezo wa kurekebisha hali ya hewa au mfumo wa vyanzo vya maji  au yenye kuhifadhi mifugo au wanyamapori.

Wakala wa Misitu Tanzania ni taasisi yenye dhamana ya usimamizi, uvunaji na usafirishaji wa mazao ya misitu, hususan mkaa, mbao, kuni, magogo, nguzo na mazao ya nyuki na jukumu lingine ni kusimamia utekelezaji wa sheria za misitu katika maeneo yaliyo chini yake.
Kutokana na jukumu hilo, Wakala kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usafirishaji  wa Nchi Kavu na Majini  (SUMATRA)  na Jeshi la Polisi  wameendelea na kampeni  ya kutoa elimu kwa wananchi  kufuata sheria na kanuni za usafirishaji halali  wa mazao ya misitu.
Aidha, Wakala pia inatoa elimu kwa wananchi  juu ya matumizi bora ya vyombo vya moto zikiwemo pikipiki za magurudumu mawili na baiskeli kutokubeba mazao hayo mazao ya misitu.
Akizungumzia suala la kusafirisha mazao ya misitu kwa kutumia pikipiki na baiskeli, Kamanda  wa Kikosi  cha Usalama barabarani, Kamishna  Msaidizi Mohamed  Mpinga  alisema kuwa ubebaji huo hauruhusiwi na ubebaji wa mazao hayo ya misitu kwa njia zisizoruhusiwa vimekuwa ni miongoni mwa vyanzo vya ajali za barabarani.
“Sheria  ya usalama barabarani, sura ya 58 sehemu ya  1 na 2 inazungumzia upakiaji wa hatari, hivyo  ni marufuku kwa dereva kupakia kupita kiasi pia inakataza ubebaji wa mizigo kiasi ambacho mwendeshaji anashindwa kuona nyuma na pia anakosa nafasi ya kukaa vizuri na hivyo kusababisha uendeshaji usio salama” anasema Kamanda Mpinga.
Kamanda huyo pia amesisitiza  kuwa sheria za usalama barabarani  zipo kwa ajili ya kulinda usalama wa dereva  na ametoa wito kwa madereva wa pikipiki  na baiskeli kuacha kubeba mizigo kupita kiasi katika vyombo hivyo.
SUMATRA ambayo ndio wenye dhamana ya wanasimamia leseni za usafirishaji  na masharti yaliyopo kisheria, imepitisha sheria ambayo inaruhusu pikipiki na baiskeli kubeba abiria mmoja tu, kinyume na hapo ni ukiukwaji wa sheria na kuhatarisha usalama wa dereva na raia wengine wanaotumia barabara.
Kaimu Mkurugenzi wa  Udhibiti na Usafiri wa Barabarani ndugu Leo Ngowi alisema kuwa kanuni za usafirishaji za mwaka 2010 zinakataza mtu yoyote kufanya biashara  ya kubeba abiria bila kuwa na leseni na dereva haruhusiwi kubeba mizigo kama magogo na mkaa.
Aliendelea kusema kuwa mamlaka haitasita kumkamata na kumfungulia mashtaka mtu yoyote ambaye anakiuka kanuni  hizo za matumizi tofauti ya msingi wa matumizi ya vyombo hivyo vya usafiri.
Profesa Dos Santos Silayo ambaye ni mtendaji Mkuu wa Wakala wa Misitu  alisema kuwa Wakala unasimamia  sheria ya misitu  namba 14 ya mwaka 2002, kifungu cha 106 pamoja na kanuni za sheria  hiyo za mwaka 2004, inayotoa maelezo na mwongozo wa uvunaji na usafirishaji wa mazao ya misitu ya mwaka 2005.
“Sheria hiyo inatoa maelekezo ya namna ya uvunaji unavyopaswa kufanywa pamoja na usafirishaji wake, ikiwa ni pamoja na kutekeleza sheria nyingine za nchi za usalama barabarani  na masharti ya leseni ya usafirishaji yanayosimamiwa na SUMATRA” alisema Profesa Silayo.
Aliongeza kusema kuwa siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la usafirishaji wa mazao ya misitu kwa kutumia pikipiki na baiskeli. Aliitaja mazao yanayosafirishwa kwa wingi kuwa ni pamoja na mkaa, mbao na nguzo ambayo kwa kiasi kikubwa yanapatikana kwa njia zisizo rasmi na wafanyabiashara wakubwa wanatumia njia hizi kukwepa vizuia vya ukaguzi.
Kwa kutumia vyombo hivyo  wafanyabiashara hao wanaweza kuingia kwenye maeneo mengi ya misitu na hivyo kusababisha  uharibifu mkubwa wa misitu na kukwepa ushuru wa Serikali uliowekwa kwa mujibu wa sheria.
Alisema kuwa usafirishaji wa mazao ya misitu kwa kutumia pikipiki na baiskeli hauruhusiwi kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi. Alitoa wito kwa kila msafirishaji na mfanyabiashara wa mazao ya misitu yanayopatikana kihalali, kutumia vyombo vinavyoruhusiwa kisheria.
Kamanda Mpinga alitoa wito kwa waendesha pikipiki  na baiskeli ambao wamekuwa na mazoea ya kupakia mazao ya misitu kutoka eneo moja kwenda lingine kiasi cha kuweza kusababisha madhara kwa watumiaji wengine wa barabara  kuacha mara moja tabia hiyo.
“Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali kwa wenye kuendeleza tabia ya kupakia mkaa na mazao mengine ya misitu, kiasi cha kuhatarisha maisha yao na watumiaji wengine wa barabara” alisema kamanda Mpinga.
Kamanda Mpinga amewataka madereva hao kuzingatia sheria na kanuni mbalimbali zilizopo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuhakikisha kuwa masuala yote yanayohusiana na usafirirshaji wa mazao hayo yanakwenda kwa mujibu wa maelekezo wanayopewa na wataalamu mbalimbali katika maeneo yao wanapoishi.
Naye ndugu Ngowi amewataka watu wote wanaotumia vyombo vya kusafirishia abiria kuacha mara moja kutumia vyombo hivyo kinyume cha matakwa ya leseni ya chombo husika.
Hivi karibuni Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania walianza operesheni ya kuimarisha utekelezaji wa sheria za usafirishaji wa mazao ya misitu hususani mkaa, kwa lengo la kuwahimiza wananchi kufuata kanuni na sheria hizo.
Akizungumza  jijini Dar es salaam hivi karibuni , Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi Endelevu ya Misitu na Nyuki nchini, ndugu Mohamed Kilongo alisema kuwa utekelezaji huo utafanyika katika mikoa yote ya Tanzania Bara na utashirikisha maofisa wa polisi, SUMATRA  pamoja na Wakala wa Misitu.
“Tathmini iliyofanyika inaonyesha kuwa pikipiki na baiskeli zinachangia uvunaji haramu na usafirishaji  wa haraka wa mazao ya misitu ambapo inakadiriwa kuwa pikipiki 20  zikisafirisha mkaa  ni sawa na lori moja la tani saba  lililojaa mkaa” alisema ndugu Kilongo.

No comments