Header Ads

Responsive Ads Here

SERIKALI YAIPONGEZA SERENGETI BOYS KWA USHINDI DHIDI YA ANGOLA,MICHUANO YA AFCON


Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe amewapongeza wachezaji wa Timu ya Taifa ya Vijana “Serengeti Boys” walimu na viongozi wao kwa ushindi wa magoli 2 –1 dhidi ya Angola jana jioni nchini Gabon.

Katika ujumbe aliompelekea Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo wa Wizara yake Bw. Yusuf Singo Omari, ambaye yuko nchini Gabon kwa fainali  za AFCON, Dkt. Mwakyembe amemwagiza Bw. Singo kuwaeleza wachezaji, walimu na viongozi wa Serengeti Boys kuwa taifa limejawa na furaha kutokana na ushindi huo na mchezo wa kiwango cha juu ulioonyeshwa na vijana hao.
Taarifa yake kamili aliyoituma Gabon mara baada ya mechi hiyo jana jioni ilisema “ushindi wa timu yetu ya Taifa ya Vijana wa magoli 2 kwa 1 dhidi ya Angola umepokewa na Watanzania wote kwa furaha isiyo na kifani na vilevile kwa ari mpya ya kuiombea na kuitakia Serengeti Boys ushindi mnono dhidi ya Niger Jumapili wiki hii”.
“Vijana wetu wameionyesha dunia kandanda safi la kiwango cha juu na wameweza kuwathibitisha watanzania wenzao dhamira ya kauli mbiu ya: GABON HADI KOMBE LA DUNIA”.
Vijana wetu wakumbuke daima kuwa kila wanapokuwa uwanjani hawapo peke yao bali na baraka za watanzania wote ambao wanafuatilia mashindano hayo kwa karibu kupitia redio, runinga, mitandao ya kijamii na magazeti. Watambue kuwa taifa zima liko nyuma yao kwa maombi ya heri na mafanikio.
KILA LA HERI SERENGETI BOYS.

Imetolewa na:
Zawadi Msalla
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo.
19/05/2017

No comments