Header Ads

Responsive Ads Here

NDIKILO -WAKULIMA WA MATUNDA WALIME KISASA ILI KUPATA SOKO NDANI NA NJE YA NCHI


viw1
Mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo, wa pili kushoto akionyeshwa namna bidhaa mbalimbali kama pilipili zinavyofungashwa katika kiwanda cha kusindika matunda cha Elven Agri co. Ltd kilichopo Mapinga Bagamoyo. 

viw2viw3
Mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo, aliyeshika ndizi, akionyeshwa hatua za uzalishaji katika usindikaji wa matunda kwenye kiwanda cha kusindika matunda cha Elven Agri co. Ltd kilichopo Mapinga, Bagamoyo. (picha na Mwamvua Mwinyi)
…………………………………………………………………………………..
Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
WAKULIMA wa matunda wametakiwa kulima kwa kutumia mbegu bora na kilimo cha kisasa ili kupata soko kwenye viwanda vinavyosindika zao hilo, ndani na nje ya nchi. 
Aidha wananchi wameshauriwa kulima kilimo kinachostahimili ukame ikiwemo mahindi,mhogo,viazi vitamu na mikunde ili kujihadhali na baa la njaa baadae
Hata hivyo wametakiwa kuhifadhi chakula wakati wa mavuno utakapofika kwani kwa kufanya hivyo itawasaidia kuwa na akiba ya kutosha.
Rai hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo, alipotembelea kiwanda cha Elven Agri company ltd kilichopo Mapinga na kiwanda cha Sayona kinachomilikiwa na kampuni MAMA ya MMI steel,kilichopo kata ya Mboga wilayani Bagamoyo.
Alieleza, wakulima wengi wanahitaji kulima kwa tija badala ya kupata hasara kwa kukosa masoko. 
Mhandisi Ndikilo alisema, kwa kutambua hilo, kuna kila sababu ya kubadilika kwa kuona umuhimu wa kulima matunda yaliyo na rutuba, bora na yanayojiuza.
“Wataalamu wa kilimo, watendaji wa halmashauri katika idara hii, mtoke maofisini muende kuwapa elimu wakulima hawa ili waweze kujifunza kulima kwa kutumia mbegu za msimu mfupi,kuweka pembejeo na kupalilia “
“Kwa kutoa elimu za mara kwa mara kwa kufuata teknolojia za kisasa, lazima waende na wakati ili waweze kunufaika kwa jasho lao “alisema mhandisi Ndikilo.
Mhandisi Ndikilo alielezea kwamba, wakulima waondokane na Kilimo cha kizamani, badala yake walime kilimo cha tija ili kujiinua kiuchumi na kimaendeleo. 
Hata hivyo alisema, kiwanda cha Elven Agri .co. ltd,na Sayona kwa sasa vitakuwa ni mkombozi kwa wakulima hao wa matunda .
Mkuu huyo wa mkoa alifafanua, kiwanda cha Elven kinahitaji tani nane na cha Sayona tani tisa kwa siku hivyo vitakuwa msaada mkubwa kwa wakulima wa matunda kimkoa na Tanzania kijumla.
Mkurugenzi mtendaji wa Elven Agri Company Ltd, Darpan Pindolia ,alisema kiwanda kwasasa kinazalisha kwa asilimia 20 pekee. 
Alibainisha, kiwanda kinajishughulisha na kusindika matunda mbalimbali kama nanasi, ndizi, maembe,pilipili na mapeasi ,kimejengwa kwa gharama za dollar mil.nne sawa na sh.bil 10,kimeanza uzalishaji mwezi uliopita.
Nae afisa uhusiano wa kampuni za MMI steel ikiwemo Sayona,Abubakar Mlawa ,alisema kiwanda cha Sayona kimefikia asilimia 70 ya ujenzi na mwezi novemba mwaka huu kinatarajia kuanza kazi.
Alieleza kiwanda hicho,kwasasa kimeajiri watu 100 wakiwemo mafundi ujenzi na kitakapoanza kazi kitaajiri watu 800.
Mlawa alisema,mahitaji makubwa ni matunda hasa maembe,nyanya na matunda mengine hivyo wakulima wa matunda wachangamkie fursa hiyo.
Kiwanda cha Sayona ni moja ya uwekezaji mkubwa mkoani Pwani,na kinalenga kugharimu dollar mil.55 sawa na sh.bil.120 katika ujenzi wake.

No comments