Header Ads

Responsive Ads Here

FURSA ZA WATANZANIA KUFUNDISHA KISWAHILI AFRIKA ZAONGEZEKA.


unnamed
Jovina Bujulu- Maelezo
Hivi karibuni, Tanzania ilitembelewa na ugeni wafanyabiashara zaidi ya 80 kutoka Afrika Kusini ambao uliongozwa na Rais wa nchi  hiyo Jacob Zuma kwa  lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili.

Ujio huo ulikuwa na nia ya kusaini makubaliano katika nyanja za biashara na uwekezaji, Bioanuwai na utalii na uchukuzi.
Makubaliano hayo ambayo  yamegawanyika katika sekta za elimu, mifugo, kilimo, madini, afya, sayansi na teknolojia na ulinzi na usalama ni kelelezo tosha  kuonyesha dhamira ya mshikamano  wa nchi hizi mbili katika  kujiletea maendeleo  kiuchumi na kijamii.
Katika eneo la sekta ya elimu ushirikiano huo utahusisha utafiti, kubadilishana uzoefu wa walimu, ambapo Serikali hizi zimeingia makubaliano yanayotoa  fursa nzuri kwa Watanzania  kwenda kufundisha lugha  ya Kiswahili  katika  taasisi za elimu zikiwemo shule  na vyuo vikuu nchini humo.
Ugeni wa Rais Zuma na ujumbe wake nchini umeleta neema kwa Watanzania kwani  watapata fursa nyingine ya ajira  nje ya nchi ambapo pia watapata fursa ya kupata uelewa mpana  wa mambo mbalimbali nchini Afrika Kusini na pia kuitangaza nchi yetu katika nyanja  kimataifa.
Akizungumzia fursa hiyo, Rais Magufuli alisema kuwa walimu hao watapelekwa nchini humo wakati wowote. Hatua hiyo inatoa fursa nyingine kwa walimu wa Kiswahili na wataalamu wabobezi wa lugha hii kujipatia ajira na pia kupata fursa ya kuitangaza lugha ya Kiswahili kimataifa.
Fursa hii ni muhimu, hivyo ni vema walimu wa Kiswahili na wataalamu waliobobea katika lugha hii wakaichangamkia ikizingatiwa hapa nchini ndiyo lugha ya Taifa na lugha inayotuunganisha ambayo pia ilitumika katika kurahisisha harakati za ukombozi wa nchi yetu.
Katika kuonyesha nia ya dhati ya kukuza lugha hii, hivi karibuni Rais Dkt. John Magufuli aliahidi kupeleka walimu wa lugha ya Kiswahili nchini Ethiopia na Rwanda. Aidha, Rais amekuwa mfano mzuri kwa kutumia lugha hii katika shughuli za Serikali akiwa hapa nchini au hata nje ya nchi.
Ndio maana mara kwa mara amekuwa akisisitiza kwa kusema anakipigia debe Kiswahili ili kiweze kuendelea kutumika katika nchi mbalimbali duniani.
Lugha ya Kiswahili ni miongoni mwa lugha zinazotumiwa na watu wengi duniani. Kwa sasa inakisiwa kuwa watumiaji wa lugha hii duniani wapatao zaidi ya milioni 120.
Wito kwa Watanzania wenye sifa, kuchangamkia fursa nyingine ya ajira ambayo sio tu itaipaisha lugha ya Kiswahili bali pia itawape heshima walimu watakaokwenda kufundisha nchini  humo.
Aidha, kwa watakaofanikiwa kwenda huko wanapaswa kuwa mabalozi wazuri wa nchi yetu kwa kutangaza mazuri ya nchi yetu, ikiwa ni pamoja na fursa mbalimbali za kuwekeza katika sekta mbalimbali ili Tanzania ifikie azma yake ya kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo 2025.

No comments