Header Ads

Responsive Ads Here

ASKOFU GADI ATOA SALAMU ZA POLE KWA WAFIWA AJALI YA KARATU


1
Na Fatma Salum,MAELEZO,Dar es Salaam
MWENYEKITI wa Kanisa la Good News For All Ministry Askofu Dkt. Charles Gadi ametoa salamu za pole kwa wafiwa na Watanzania wote walioguswa na msiba wa wanafunzi 32, walimu wawili na dereva wa shule ya Msingi Lucky Vincent iliyotokea Karatu Mkoani Arusha wiki iliyopita.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Askofu Gadi alisema kuwa kanisa lake linaungana na familia za marehemu hao kuomboleza msiba huo mkubwa ulioacha pengo na simanzi kwa familia na taifa kwa ujumla.
Askofu Gadi pia ameipongeza Serikali ya Rais Dkt. John Magufuli kwa kushirikiana bega kwa bega na familia za wafiwa na wananchi wa Mkoa wa Arusha katika kuomboleza msiba huo jambo ambalo limewaunganisha Watanzania na kuleta faraja kwa familia zilizopoteza watoto wao.
“Tunaipongeza Serikali yetu ya Mhe.Rais Dkt. John Magufuli kwa jinsi ilivyouchukulia msiba huu kwa uzito mkubwa. Tumeguswa sana jinsi Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu alivyoshiriki kwenye kuaga miili ya watoto hao.” Alisema Askofu Gadi.
Aidha Askofu Gadi alieleza kuwa wanaunga mkono wito wa Serikali kwa madereva
wote nchini kuacha kuendesha gari mwendo kasi na kuzingatia sheria za usalama barabarani.
Katika hatua nyingine Askofu Gadi amepongeza jitihada za Rais Magufuli kwa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ambayo ameizindua hivi karibuni ikiwemo ujenzi wa barabara za juu (fly overs), reli mpya ya kisasa (standard gauge) na miradi mingine.
“Tunaamini kwa kasi hii, Rais Magufuli na Serikali yake watailetea nchi yetu maendeleo makubwa ya kupigiwa mfano hivyo nawaomba Watanzania wenzangu tuendelee kumuombea na tufanye kazi kwa bidii kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu.” Aliongeza Askofu Gadi.
Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Askofu Gadi aliongoza maombi ya kumuomba Mungu mvua iache kunyesha mkoani Dar es Salaam na ukanda wa pwani badala yake Mungu aielekeze kwenye mikoa mingine ambako inahitajika kwa ajili ya kilimo na shughuli nyingine.

No comments