Header Ads

Responsive Ads Here

TAARIFA KUTOKA JESHI LA POLISI MKOANI MBEYA


PICHA-RPC-MBEYA

Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu. Mafanikio yaliyopatikana katika Misako ni kama ifuatavyo:-

KUKAMATWA KWA MTU ANAYEJIFANYA MTUMISHI WA BENKI YA CRDB – MBEYA.
Mnamo tarehe 25.04.2017 majira ya saa 16:50 jioni huko katika Benki ya CRDB Tawi la Mwanjelwa iliyopo Kata ya Mwanjelwa, Tarafa ya Iyunga, Jiji na Mkoa wa Mbeya, Mtu mmoja anayefahamika kwa jina la ISAYA MWAKEYE [29] Mkazi wa CCM Ilomba hapa Jijini Mbeya anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kosa la kujifanya mtumishi wa Benki ya CRDB kwa cheo cha afisa mikopo wa Benki hiyo.
Aidha mtuhumiwa alikuwa akionekana mara kadhaa katika Chuo Kikuu cha Mzumbe Tawi la Mbeya na alikuwa akihudhuria masomo kama wanafunzi wengine na anadaiwa kuwa alikuwa anaishi Chuoni hapo.
Mtuhumiwa alikamatwa na watumishi wa Benki ya CRDB Tawi la Mwanjelwa akiwa ndani ya Benki hiyo akiwa amevaa T-Shirt yenye nembo ya CRDB huku akijitambulisha kuwa yeye ni mtumishi wa Benki na Tawi hilo. Aidha baada ya mtuhumiwa kuhojiwa na kupekuliwa alikutwa na kitambulisho cha CRDB Tawi la Mwanjelwa, Kadi za ATM zenye namba 61410010485 – NMB Chap Chap Tawi la Tukuyu, Akaunti namba 6101610146 SEMBELE G. S Tawi la Mbalizi Road, Akaunti namba 0152300144500 CRDB na SHEBAMILES ET 00014623663 MWANGOSI GEOFREY na kitambulisho cha Chuo cha TIA Mbeya chenye namba ya usajili BA 4209.
Pia mtuhumiwa alikutwa na karatasi ambazo amezitengeneza na kuzipaka rangi na kuwa na muonekano wa noti ya Tshs elfu kumi. Mtuhumiwa anashikiliwa kwa mahojiano zaidi. Aidha mara baada ya upelelezi kukamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
KUPATIKANA NA NYARA ZA SERIKALI – MENO YA TEMBO NA SILAHA BUNDUKI MOJA.
Mnamo tarehe 24.04.2017 majira ya saa 16:20 jioni huko Kijiji cha Lyangadupa, Kata na Tarafa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Askari wa TANAPA walifanikiwa kuwakamata watu wawili waliofahamika kwa majina ya 1. SUPARIANO JOJI [26] Mkazi wa Lyangadupa na 2. JOSEPH NGADUPA [59] Mkazi wa Imalilo – Songwe wakiwa na Meno mawili ya Tembo.
Watuhumiwa walikamatwa wakiwa wanauza meno hayo baada ya kupata taarifa za siri na kuweka mtego uliofanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao. Aidha katika mahojiano, watuhumiwa hao walikiri kuhusika na mauaji ya Tembo kadhaa. Pia watuhumiwa baada ya kuhojiwa zaidi waliweza kuonyesha mahali walipoficha silaha moja bunduki aina ya Gobole na risasi 12 za golori ambayo huitumia kuwindia.
Watuhumiwa ni wawindaji haramu juhudi zinafanyika ili kufanikiwa kubaini na kuwakamata watuhumiwa wengine wanaohusika na mtandao wa ujangiri/wawindaji haramu.
WITO:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishina wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI anatoa wito kwa vijana na jamii kwa ujumla kuacha tamaa ya kutaka kujipatia mali kwa njia za udanganyifu na utapeli kwani ni kinyume cha sheria na kamwe Jeshi la Polisi halitavumilia aina yoyote ya uhalifu. Aidha Kamanda KIDAVASHARI anatoa wito kwa wananchi kuwa makini wanapofanya shughuli za kibenki ili kuepuka matapeli. Pia anatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
                                               Imesainiwa na:
[DHAHIRI A. KIDAVASHARI – DCP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.

No comments