Header Ads

Responsive Ads Here

RAS TABORA AWAONYA MADED KUTUMIA FEDHA KWA MIRADI ILIYOKUSUDIWA


20160831_092703
Na Tiganya Vincent, RS-Tabora
 
Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Dkt. Thea Ntara amewaagiza Wakurugenzi Watendaji (MA-DED) na Wahandisi wote wa Maji katika Halmashauri zote nane ya Mkoa huo kuhakikisha kuwa wanasimamia na kufuatilia vema matumizi ya fedha za ufufuaji wa miradi ya maji vijijini kwa kutumia milioni 20 walizopata kila moja.
 
Dkt. Ntara alitoa kauli hiyo jana mjini Tabora wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa Watendaji hao kuhakikisha wanashinda vjijini kwa lengo la kutaka miradi itajengwa au kufufuliwa ilingane na thamani ya fedha iliyotolewa na Serikali .
 
Alisema kuwa kila Halmashauri mkoani humo imepata shilingi milioni 20 za ufufuaji wa miradi ya maji vijijini ni vema wakatumia muda kuisimamia na kuhakikisha inatoka na ubora uliokusudiwa.
 
“Nawaagiza washinde vijijini kuhakikisha kuwa ujenzi wa miradi inazingati ubora na inasaidia kuondoa kero kwa wananchi na sio kujenga miradi ambayo haidumu, hilo jambo sitakubali” alisisitiza Dkt. Ntara.
 
 
Katibu Tawala huyo wa Mkoa aliuagiza Uongozi wa Halmashauri ya Sikonge uliopata shilingi milioni 625 ambazo imepata nje ya zile milioni 20 kutumia fedha hizo kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Awamu wa Bwawa.
 
Alisema kuwa ni vema kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo na Wahandisi wake wakamusimamia kwa karibu mtu aliyepewa mradi huo ili akamilishe kwa haraka na kwa kiwango bora.
 
Dkt. Ntara alisema kuwa kwa upande wa Halmashauri ya Nzega ambao nao wamepata milioni 25 kwa ajili ya ufuatiliaji nje ya zile za ufufuaji wa miradi ya maji vijijini kutumia fedha hizo katika kuhakikisha wanafuatilia miradi ili ikamilike.
 
Katika hatua nyingine Katibu Tawala huyo Mkoa wa Tabora ametoa onyo kwa Wakurugenzi Watendaji  wa Halmashauri zote kuhakikisha wanafanya malipo kulingana vikao halisi vya siku za Mabaraza ili kuepuka udanganyifu.
 
Alisema kuwa sio vema kwa Ma-DED kuliwalipa Wajumbe zaidi ya siku walizokaa kihalali na kuongeza kuwa kufanya hivyo ni ubadhirifu wa fedha za wananchi.
 
“Napenda kuwakumbusha Wakurugenzi wote wa Halmashauri kulipa posho kulinga na siku za vikao na sio kikao kinafanyika siku moja wajumbe wanalipwa posho za siku tatu au nne wakati siku nyingine hawakuwa na kikao ..huu ni ubadhirifu wa fedha za wananchi na Serikali hii inapiga marufuku vitendo hivyo” alisisitiza Dkt. Ntara.
 
Alisema kuwa ili kukabaliana na tatizo hilo amewaagiza Wakurugenzi wote watendaji wa Halmashauri za Mkoa wa Tabora kupeleka kwake ratiba ya shughuli za vikao vya Mabaraza ya Madiwani, Ajenda zitazojadiliwa na siku za vikao.
 
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa posho inayolipwa kweli ni halali na sio kutumia ujanja kutumia fedha za umma kwa maslahi binafsi.

No comments