Header Ads

Responsive Ads Here

MVIWATA WAIOMBA SERIKALI KUUNDA SHERIA KUWABANA WAFANYABIASHARA WA UFUTA


ufuta  
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Mtandao wa Vikundi vya Wakulima nchini (MVIWATA) umeiomba Serikali kutunga sheria ndogo ndogo zitakazowabana wafanyabiashara wa zao la ufuta ili wakulima wapate faida ya uzalishaji wa zao hilo.

Maombi hayo yamebainishwa hivi karibuni na Afisa Masoko kutoka MVIWATA, Acquiline Wamba wakati wa warsha ya uboreshaji wa matumizi ya vipimo sahihi katika biashara ya mazao ya kilimo iliyofanyika mkoani Dodoma.
Bi. Acquiline amesema Serikali inatakiwa kuchukua hatua madhubuti kwa kuweka sheria kali dhidi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kwani Sheria hizo  zitawasaidia kuwapa maelekezo ya namna ya kuweka vipimo sahihi kwenye mazao ili kuongeza ushindani kwenye biashara.
“Wafanyabiashara wasio waaminifu wamekua ni chanzo cha kukwamisha soko la nje kwa kupeleka mazao yenye uchafu nje ya nchi, hii sio sahihi ndio maana tunaomba Serikali itusaidie” alisema Bi. Acquiline.
Aliongeza kuwa ili kuboresha soko la nje la zao la ufuta Serikali inatakiwa kuhakikisha panakwepo na mazingira wezeshi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mazao yanayoenda nje ni masafi.
Aidha, Bi. Acquiline alifafanua kwamba kuwabana wafanyabiashara wa zao hilo kutumia vipimo sahihi vya mizani itasaidia kukomesha  wafanyabiashara wanaowaibia wazalishaji hao kwani lengo halisi la kuweka mizani ni kupunguza tabia ya baadhi ya wafanyabiashara kuongeza mchanga kwenye zao la ufuta kwa lengo la kuongeza uzito.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Danford Chisomi alisema kuwa Halmashauri bado haijawa na mizani ya mazao kutokana na ufinyu wa bajeti hivyo aliahidi kushiriki katika kutatua changamoto hizo.
“Halmashauri itatafuta nafasi ya kuweka mizani pamoja na kuunda sheria mpya ndogondogo za kuwadhibiti wafanyabiashara wa zao hilo”, alisema Chisomi.
Akiongea katika warsha hiyo, mzalishaji wa ufuta Wilayani Bahi, Fikiri Bernard, alisema kukosekana kwa mizani katika Halmashauri hiyo kunaathiri moja kwa moja jitihada za wazalishaji pamoja na kusababisha upotevu wa mapato kwa halmashauri hiyo.
“Vipimo vingi vinavyotumiwa na wafanyabiashara huwa haviko sahihi kwa sababu havijahakikiwa na Mamlaka husika kwa matumizi ya biashara hivyo wafanyabiashara wamekua wakitumia mwanya huo wa ukosefu wa mizani kuweka vipimo vyao wenyewe vya kununulia zao la ufuta,” alisema Bernard.
Ameongeza kuwa Halmashauri hiyo imekua ikipoteza mapato mengi kwa kushindwa kukusanya ushuru kutokana na kuwepo kwa wafanyabiashara wasio waaminifu wanaopenyeza mazao yao bila kulipa ushuru.
Vile vile, mkulima huyo ameiomba Halmashauri kutenga vituo mbalimbali vya kupimia mazao kwa ajili ya kupata vipimo sahihi vya mazao ili kuepuka kuwaibia wakulima.

No comments