Header Ads

Responsive Ads Here

MOI YAJIPANGA KUONGEZA MUDA WA KUTOA HUDUMA


4Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) imejipanga kuongeza muda wa kutoa huduma za afya ili kuweza kutoa tiba kwa wagonjwa wengi pamoja na kuongeza mapato yatakayotumika kuendeshea taasisi hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dkt. Respicious Boniface ameyasema hayo leo wakati wa kikao cha 4 cha Baraza la 3 la wafanyakazi wa taasisi hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Iddy Nyundo ulipo Jijini Dar es Salaam.
Dkt. Boniface amesema kuwa bajeti ya Serikali pekee haiwezi kujitosheleza hivyo menejimenti na wafanyakazi wa taasisi hiyo wana wajibu wa kutafuta vyanzo vingine vya halali vitakavyoiwezesha taasisi kujiendesha kama ilivyokuwa awali.

“Katika taasisi yetu wateja wetu ni wagonjwa hivyo tunatakiwa kuimarisha huduma zetu ili tuweze kuwahudumia wagonjwa wengi zaidi, tumepanga kuongeza muda wa kutoa huduma kwa wagonjwa wa kawaida na wanaohitaji upasuaji, kuongeza vifaa vya maabara pamoja na wodi za wagonjwa ikiwa ni njia ya kuongeza mapato ya taasisi,” alisema Dkt. Boniface.
Mkurugenzi Boniface ameongeza kuwa ni muhimu wafanyakazi kufanya kazi kwa bidii kwa kutafuta njia mbadala za kujiinua kuliko kulalamika hivyo ni vema kutumia mfumo wa ufanyaji kazi wa sekta binafsi na  kuweka timu bora kuanzia ngazi ya chini hadi ya juu kwa ajili ya mapambano yatakayopelekea kuboresha huduma na mapato.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini wa MOI, Prof. Bakari Lembariti amesema kuwa ili kuleta mageuzi makubwa ndani ya taasisi na kuhakikisha taasisi inafanya vizuri ni wajibu wa kila mfanyakazi kuhakikisha MOI inasimama kwa kujitoa kufanya kazi kwa moyo.
“Pamoja na changamoto zote mlizokuwa nazo, nawashauri kuacha lugha chafu kwa wagonjwa,utoro kazini pamoja na rushwa kwani vitendo hivyo viovu ndivyo vinavyopelekea kupunguza wateja na kupeleka kupunguza kipato,”alisema Prof. Lembariti.
Aidha, amewataka wafanyakazi kuzipitia kanuni za utumishi wa umma na kuzielewa ili wafanye kazi kulingana na kanuni hizo na kwa atakaepuuzia achukuliwe hatua stahiki.
Taasisi ya MOI imeanzishwa mnamo mwaka 1996 ikiwa na lengo la kutoa huduma bora za afya kwa wagonjwa wa mifupa, upasuaji wa uti wa mgongo na mishipa ya fahamu.

No comments